Ndanda

Ugonjwa wa figo

Ukubwa wa tatizo la ugonjwa sugu wa figo nchini Tanzania unazidi kuongezeka siku hata siku na inaelezwa kwamba kuna ongezeko la 7% mpaka 15% kutokana na tafiti zilizofanyika katika jamii. Hivyo basi kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza jitihada za kuzuia,kutambua ugonjwa huu wa figo hasa vijijini. Kwa hiyo mwaka 2018 uongozi wa hospitali ya Ndanda uliamua kuanzisha kliniki ya figo na huduma ya kusafisha damu kwenye kituo chetu. 

Dayalisisi ya tumbo

Mradi  wa kusafishwa figo kwa njia ya tumbo ulifanyika kwa mara ya kwanza katika hospitali yetu kwa ushirikiano na Dr. Kajiru Kilonzo, daktari bingwa wa figo kutoka hospitali ya KCMC ambaye aliambatana na Mrs. Willina Mosha,muuguzi wa dayalisisi kutoka KCMC mnamo mwezi Oktoba 2018, hadi mwisho wa mwaka 2021,wagonjwa 21 wametibiwa kwa kusafisha figo kwa njia ya tumbo. Wengi wao walikuwa watoto waliopata tatizo la figo ghafla na wengi wao wamepona. Wagonjwa wakubwa wenye shida hii sugu ya mafigo pia wametibiwa vizuri na mmoja alifanikiwa kupandikizwa figo Hospitali ya Taifa Muhimbili mnamo mwezi Julai 2019.

Kliniki ya ugonjwa wa figo

Kliniki hii ilianza rasmi Januari 2020 ambapo tunatoa huduma kila wiki na Daktari wa matibabu (MD). Mara moja kwa mwezi Daktari bingwa wa figo anakuja kuwahudumia wagonjwa wa nje wenye magonjwa ya figo pamoja na wagonjwa wa dayalisisi. Wagonjwa waliopata ugonjwa wa figo ghafla,na wagonjwa walio na ugonjwa sugu wa figo uchunguzwa na kutibiwa kulingana na miongozo husika.Wagonjwa walio na ugonjwa wa figo wa hatua ya mwisho wanapata huduma ya uchujaji damu kama daraja la upandikizaji wa figo kama matibabu halisi.

Dayalisisi ya damu

Huduma hii ya dayalisisi inapatikana katika hospitali yetu tangu mwezi wa tisa 2020. Tunazo mashine 10 za kisasa ambazo zimesanikishwa,nyingi zikiwa ni Fresenius 5008S. Timu yetu ya dayalisisi inajumuisha daktari mmoja (MMED), MD mmoja,wauguzi sita wa dayalisisi na mhudumu mmoja wa afya. Idara inasimamiwa na mtaalam wa magonjwa ya figo Dr Onesmo Kisanga ambaye anatutembelea mara moja kila  mwezi. Kati ya wagonjwa 30 na 40 walio na ugonjwa wa figo wa hatua ya mwisho wanakuja mara kwa mara kwa kupata huduma ya dayalisisi,wengi wao wanakuja mara tatu kwa wiki.   

Maono yetu

Utoaji wa huduma bora zaidi utakaokidhi mahitaji thabiti na endelevu kwa mgonjwa husika kwa namna ya huruma na heshima kubwa kutoka kwa wataalamu wetu.

Dhamira yetu

Kuwa kituo bora zaidi katika utoaji huduma hii ya kibobezi kusini mwa Tanzania na kitaifa kwa ujumla.