Ndanda

CT Scan

Mafunzo ya Neonatolojia na  Ultrasound

Kuanzia tarehe 23/11/2023 hadi tarehe 27/11/2023,  Dr. Christian Schmidt, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto na  Irene Schmidt mke wake muuguzi aliyebobea katika taaluma ya watoto wachanga kutoka Jumuiya ya Ujerumani ya madaktari wa watoto wa kitropiki na afya ya kimataifa ya watoto (GTP) walitembelea hospitali yetu. Wametoa mafunzo juu ya utunzaji mkubwa wa watoto wachanga,uchunguzi wa dharura wa utrasound na moyo.Madaktari na wauguzi wa idara zetu za watoto na NICU pamoja na hospitali za jirani ndani ya mikoa ya Mtwara na Lindi wameshiriki katika mafunzo hayo.

 

Saa za asubuhi madaktari na wauguzi walifundishwa kwa pamoja juu ya misingi ya Neonatolojia kama ufufuaji wa watoto wachanga, tiba ya oksijeni (CPAP), ulishaji na udhibiti wa maji. Baada ya mapumziko mafupi ya chai wauguzi walipata mafunzo ya vitendo kuhusu huduma ya NICU, Madaktari wakiendelea na mafunzo ya uchunguzi wa utrasound na echocardiography. Utumiaji wa utrasound ya uhakika na echocardiography huwezesha madaktari kutambua dharura na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo katika hatua ya awali. Baadhi ya watoto wanaweza kupewa rufaa ya kufanyiwa upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,wengine wanaweza kusimamiwa kwa matibabu kwa taratibu. Wataalamu wetu waandamizi wametoa mafunzo bora bila malipo kwa manufaa  ya wakazi wa kanda ya Kusini mwa Tanzania.