Ndanda

Siku ya Figo Duniani

Siku ya figo Duniani 2022,  uchunguzi wa  ugonjwa wa figo kwa jamii ulitolewa katika kituo chetu  tarehe 12 Machi. Matangazo ya mabango,redio na kupitia kipaza sauti yalikuwa siku moja kabla, katika vijiji vyote vinavyoizunguka Ndanda.Uchunguzi huo ulitolewa bure kwa raia wote walio zaidi ya miaka 18. Shinikizo la damu, uzito wa mwili na urefu vilirekodiwa. Wateja wote walipokea uchunguzi wa mkojo na kipimo cha sukari.

Uchunguzi ulianza saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana na wafanyakazi wetu 20 kama ilivyopangwa.  Jumla ya wagonjwa 172 walikuja kuchunguzwa, wenye umri kuanzia miaka 21 hadi 83. Wagonjwa 65 sawa na asilimia 38 waligundulika wana shinikizo la damu, wagonjwa 11 sawa na asilimia 6 walipatikana kuwa na protini kwenye mkojo kama ishara ya kuathirika kwa figo na wagonjwa 8 sawa na asilimia 3 walikuwa na maambukizo ya mfumo wa mkojo. 58 sawa na asilimia 34 ya wagonjwa walikutwa na uzito uliopitiliza na wagonjwa 11 sawa na asilimia 5 waligundulika kuwa na viwango vya juu vya sukari kwenye damu. Wagonjwa wote waliopatikana na majibu yasiyo ya kawaida walishauriwa wapate uchunguzi zaidi na matibabu yake. Matokeo yanathibitisha kwamba kuna kiwango kikubwa cha maambukizi ya shinikizo la damu, ugonjwa wa figo na kisukari kwa watu wanaozunguka kituo chetu na wengi wao bado hawajagundulika na kutibiwa.