Ukubwa wa tatizo la ugonjwa sugu wa figo nchini Tanzania unazidi kuongezeka siku hata siku na inaelezwa kwamba kuna ongezeko la 7% mpaka 15% kutokana na tafiti zilizofanyika katika jamii. Hivyo basi kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza jitihada za kuzuia,kutambua ugonjwa huu na matibabu ya ugonjwa wa figo hasa vijijini. Mwaka 2018 uongozi wa hospitali ya Ndanda uliamua kuanzisha kliniki ya figo na uchujaji damu kwenye kituo chetu.
Kliniki yetu inatoa huduma kila mwezi na daktari bingwa wa magonjwa ya figo kutoka Dar Es Salaam. Wagonjwa waliopata ugonjwa wa figo ghafla na sugu uchunguzwa na kutibiwa kulingana na miongozo husika. Wagonjwa walio kuwa hatua ya mwisho wanapata huduma ya uchujaji damu kama daraja la upandikizaji wa figo kama matibabu halisi.
Huduma ya uchujaji damu inapatikana katika hospitali yetu tangu mwezi wa tisa mwaka 2020. Mashine 8 za kisasa (Fresenius 5008S) zimesanikishwa ndani ya chumba cha uchujaji damu, mashine moja imewekwa chumba cha walio na maambukizi na moja chumba cha wagonjwa mahututi. Timu yetu inajumuisha daktari bingwa (MMED) daktari mmoja, wauguzi 6 wa uchujaji damu na muhudumu wa afya mmoja. Idara inasimamiwa na daktari bingwa wa figo kutoka Dar Es Salaam (Dr Onesmo KIsanga) anatutembelea mara moja kwa mwezi. Kati ya wagonjwa 30 na 40 walio na ugonjwa wa figo wa hatua ya mwisho wanakuja mara kwa mara kupata huduma ya uchujaji damu,wengi wao wanakuja mara tatu kwa wiki.
Mradi wa uchujaji wa figo kwa njia ya tumbo ulifanyika katika hospitali yetu kwa ushirikiano wa daktari bingwa na muuguzi wa uchujaji damu wote kutoka Kilimanjaro (Dr Kajuru Kilongo na Bi Willina Mosha) mwezi wa kumi 2018. Hadi kufikia mwisho wa mwaka 2023, wagonjwa 27 wametibiwa kwa njia hii ya uchujaji wa figo kwa njia ya tumbo. Wengi walikuwa watoto waliopata tatizo la figo ghafla na wengi wao wamepona. Wagonjwa wakubwa wenye shida hii sugu ya mafigo pia wametibiwa vizuri na mmoja alifanikiwa kupandikizwa figo Hospitali ya Taifa Muhimbili mwezi wa saba 2019.