Mnamo tarehe 13.9.2024, kwa mara ya kwanza katika hospitali yetu, wagonjwa walipatiwa matibabu ya Tiba Chemia. Takriban wiki moja mapema, tulipokea kibali cha serikali kwa ajili ya njia hii ya matibabu.
Hii ina maana kuwa sasa wagonjwa wenye saratani wanaweza kutibiwa kwa ufanisi katika hospitali yetu, ilhali awali huduma hii ilikuwa inapatikana tu Dar Es Salaam na sehemu za Kaskazini mwa Tanzania.
Timu yetu inajumuisha daktari Bingwa mmoja wa saratani (oncologist), Daktari mmoja (MD), wauguzi watatu, na mfamasia mmoja. MD, wauguzi, na mfamasia wamepokea mafunzo maalum kwa ajili ya tiba hii.
Wodi yetu mpya ya Tiba Chemia inakidhi mahitaji yote. Dawa zinaandaliwa na mfamasia kwenye kabati maalum ya usalama wa kibaiolojia na kupelekwa kwenye chumba cha matibabu kwa njia fupi. Huko zinawekewa wagonjwa kwa muda wa hadi saa kadhaa, wakati huo wanaweza kukaa au kulala kwa starehe kwenye viti maalum. Pia kuna chumba cha kusajili wagonjwa, eneo la kusubiri, na chumba cha daktari kwa ajili ya ushauri wa wagonjwa.
Katika wiki ya kwanza, wagonjwa 15 tayari wamepatiwa ushauri na daktari wetu wa saratani na tuliweza kutoa Tiba Chemia kwa wagonjwa wawili.
Kwa kuwa sisi ni kituo pekee katika sehemu ya Kusini mwa Tanzania kinachotoa huduma hii, tunatarajia idadi kubwa ya wagonjwa kuripoti katika wiki na miezi ijayo.