Chuo cha Uuguzi Ndanda ni sehemu ya Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Benedikto Ndanda. Chuo hutoa mafunzo ya stashahada katika uuguzi na wakunga inayolenga kutatua tatizo la upungufu wa rasilimali watu katika sekta afya nchini.
Chuo cha Uuguzi Ndanda kilianza mnamo mwaka 1930 na Sr. Dr. Theckla Stinnebeck OSB kwa kozi ya miaka minne ya ugawaji dawa. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia mnamo 1939 shule hii ilibidi kufungwa.
Mnamo 1945, kozi ya miezi 18 kwa Wakunga wa vijiji ilianza na mnamo 1950 Wizara ya Afya iliruhusu kuanza mafunzo ya miaka 2 kwa Wakunga. Mnamo 1965 kituo cha mafunzo ya uuguzi kilianza kutoa kozi ya miaka mitatu kwa wauguzi wa daraja B. Tangu kuanzishwa kwake, shule hiyo ilitoa mafunzo ya elimu ya pamoja. Mnamo 1970 mafunzo ya miaka miwili kwa Wakunga yalisitishwa, kuanzia hapo na kuendelea, wauguzi wa daraja B walipata mafunzo kama Wakunga. Mnamo 1983, kozi ya awali ya mwaka mmoja kwa Uuguzi ilianzishwa ambayo ilisitishwa mnamo Juni 1993. Mnamo Septemba 1994 kozi ya diploma katika Uuguzi ilianza.
Mnamo mwaka 2012 kozi ya Uuguzi ngazi ya cheti ilianzishwa. Mnamo Machi 2013, kozi ya miaka 2 ilianzishwa kwa ajili ya wauguzi wa ngazi ya cheti kusoma na kupata stashahada kupitia masomo ya masafa. Kwa sababu ya mabadiliko ya mtaala wa uuguzi juu ya sifa za kuingia, kozi ya cheti ilisitishwa mnamo 2017. Mnamo Septemba 2018 kozi ya mwaka mmoja kwa wauguzi wenye astashahada tuzo ya stashahada katika uuguzi na wakunga ulianzishwa.