Ugonjwa wa Saratani kwa sasa ni chanzo kikuu cha vifo nchini Tanzania baada ya ugonjwa wa moyo na matatizo wakati wa kuzaliwa. Hadi sasa kuna vituo sita pekee vya kutibu magonjwa ya saratani Tanzania. Kwa upande wa kusini mwa Tanzania matibabu hayo hayapatikani ndani ya umbali wa kilomita mia tano kuzunguka hospitali yetu. Kuna matibabu ya aina tatu : Upasuaji, Tibakemia na Mionzi. Kwa upande wa utumiaji wa Mionzi unahitaji miundo mbinu ya gharama kubwa. Hivyo wagonjwa wengi wanaweza kusaidiwa kwa urahisi na matibabu ya upasuaji na tibakemia. Mradi unalenga kuanzisha kitengo cha kuandaa Tibakemia na kutoa huduma kwa wagonjwa husika.
Wodi maalum inahitajika kwa kuandaa na kutoa tibakemia baada ya kuagizwa na daktari bingwa wa Saratani, dawa zitatayarishwa na mfamasia katika chumba maalumu. Kutoka hapo dawa huletwa moja kwa moja chumba cha matibabu ambako wagonjwa watapatiwa drip za dawa kwa masaa kadhaa wakiwa wamekaa au kulala kwenye viti maalumu vya kutolea dawa. Sehemu ya kusubiri wagonjwa, mapokezi, chumba cha daktari na vyumba vingine pia vinahitajika. Kwa mahitaji hayo hospitali yetu ya Ndanda tunaweza kukarabati jengo lisilotumika na kununua baadhi ya vifaa. Daktari bingwa wa magonjwa ya Saratani kutoka Dar es salaam atakuwa anatutembelea mara kwa mara kwa ajili ya kuchunguza wagonjwa na kuagiza matibabu kulingana na miongozo ya sasa. Tunatarajia kuanza ujenzi mwezi wa sita mwaka 2023 na kumaliza mradi huu robo ya tatu ya mwaka 2023.